1Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.
2Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.
3Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema: “Bwana Mungu Mwenyezi, matendo yako ni makuu na ya ajabu. Njia zako wewe ni za haki na za kweli, Mfalme wa nyakati zote!
4Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu. Mataifa yote yatakuja na kuabudu mbele zako, kwa kuwa matendo yako ya haki yamedhihirishwa.”
5Baada ya haya nikatazama, nalo hekalu, la hema la Ushuhuda, lilikuwa limefunguliwa mbinguni.
6Ndani ya lile hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ingʼaayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao.
7Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele.
8
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0 (creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0).