1Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi; nitaweka lijamu kinywani mwangu wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.”
2Lakini niliponyamaza kimya na kutulia, hata pasipo kusema lolote jema, uchungu wangu uliongezeka.
3Moyo wangu ulipata moto ndani yangu, nilipotafakari, moto uliwaka, ndipo nikasema kwa ulimi wangu:
4“Ee Bwana, nijulishe mwisho wa maisha yangu na hesabu ya siku zangu; nijalie kujua jinsi maisha yangu yanavyopita upesi.
5Umefanya maisha yangu mafupi kama pumzi; muda wangu wa kuishi ni kama hauna thamani kwako. Maisha ya kila mwanadamu ni kama pumzi.
6Hakika kila binadamu ni kama njozi aendapo huku na huko: hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili; anakusanya mali nyingi, wala hajui ni nani atakayeifaidi.
7“Lakini sasa Bwana, nitafute nini? Tumaini langu ni kwako.
8Niokoe kutoka kwenye makosa yangu yote, usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.
9Nilinyamaza kimya, sikufumbua kinywa changu, kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0 (creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0).
10Niondolee mjeledi wako, nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako.
11Unakemea na kuadhibu wanadamu kwa ajili ya dhambi zao; unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo: kila mwanadamu ni kama pumzi tu.
12“Ee Bwana, usikie maombi yangu, usikie kilio changu unisaidie, usiwe kiziwi kwa kulia kwangu. Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni, kama walivyokuwa baba zangu wote,
13Tazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena kabla sijaondoka na nisiwepo tena.”